NEMC yaingia mkataba kukusanya taka ngumu
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), limesaini wa ushirikiano na Kituo cha Sayansi na Mazingira (CSE), utakaosaidia baraza hilo kuboresha ukusanyaji wa taka ngumu katika maeneo mbalimbali hasa majiji. Mkataba huo umesainiwa leo Jumatatu, Januari 23, 2023 kati ya Mkurugenzi mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka na Mkurugenzi Mtendaji wa CSE chenye makazi yake nchini India. Hafla hiyo ilikwenda sambamba na mjadala wa siku tatu wa kujadili masuala ya taka ngumu. Katika maelezo yake, Dk Gwamaka amesema taka ngumu bado changamoto sio Tanzania pekee bali katika mataifa mbalimbali, ndio maana shughuli hiyo imehudhuriwa na wawakilishi wa mataifa ya Rwanda, Msumbiji, Ethiopia, Ghana, Zambia Kenya, Uganda na Eswatin. Amesema CSE wamekwenda mbali zaidi hasa katika teknolojia ya ukusanyaji wa taka ngumu, akisema kupitia mkataba watapata uzoefu wa kukabiliana na changamoto hiyo na namna ya kutengeneza mifumo ya kutenganisha taka hizo baada ya kukusanywa hadi kusafirishwa. "NEMC na CSE tunakusudia kujengeana uwezo na uzoefu ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti zinazohusiana na miji yetu katika ukusanya wa taka, pia kubadilisha uzoefu ikiwa ni pamoja wataalamu wetu kubadilisha mafunzo au kutembea nchi nyingine kujionea. "Pia kujaribu kuzipa nguvu miji au halmashauri za wilaya ili zisimamie uwezo wa kupata teknolojia na uzoefu kisha kupata tafiti za pamoja za kupunguza taka ngumu kwenda katika madampo ili miji iendelee kuwa safi," amesema Dk Gwamaka. Kwa mujibu wa Dk Gwamaka, mkataba huo ni miaka mitatu, lakini kuna uwezekano wa kuurefusha zaidi ili kuzipa nguvu mamlaka za Serikali za mitaa katika kukabiliana na ukusanyaji wa taka kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa CSE, Anumita Chowdhury amesema ushirikiano huo ni muhimu kufahamu na kuzingatia changamoto za kimazingira zinazoambatana na mabadiliko ya mipango na uchafuzi hali ya hewa. "Leo India na Tanzania tunajaribu kutafuta suluhisho la changamoto zetu kwa kufahamu nini kinahitajika katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira usiokua na gharama kubwa ambapo tutaweza kufanikisha kwa uwezo wetu. "Mkataba huu umejikita katika kusaidiana na kujifunza kutoka pande zote mbili kwenye usimamizi wa taka ngumu huku tukifahamu kwamba miji yetu inakua kwa haraka," amesema Chowdhury. Amesema taka ni rasirimali ambazo zinahitaji kurejeshwa tena na kuchangia maendeleo, akisema kupitia ushirikiano huo pande zote mbili namna nyumba itakavyopunguza matumizi ya plastiki na taka kukusanywa na kufanywa bidhaa. "Kama tulivyoona India ambapo taka zutumika kutengeneza biogas, hivyo tunaweza pia kutumia njia kama hii Tanzania ili kuondoa madampo," amesema.
